Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wahitaji dola bilioni 1 kwa shughuli za misaada Sudan Kusini

UM wahitaji dola bilioni 1 kwa shughuli za misaada Sudan Kusini

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa huduma za kibinadamu Sudan Kusini yamesema yatahitaji dola bilioni 1.1 za kimarekani ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yanayozidi kuongezeka nchini humo mwaka ujao wa 2013.

Afisi ya mratibu mkuu wa misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa idadi kubwa ya watu Sudan Kusini bado wamo hatarini kwa sababu za kiusalama, kuhama makwao, uhaba wa chakula, magonjwa na mafuriko.

Kwa mujibu wa OCHA, yapata raia milioni 4.6 wa Sudan Kusini watahitaji aina fulani ya misaada hapo mwakani, huku nusu ya idadi hiyo wakihitaji misaada ya chakula. Jens Laerke ni msemaji wa OCHA mjini Geneva

Ni kiasi kikubwa mno cha fedha, lakini shida iliyopo pia ni kubwa mno. Tuna asilimia 40 ya idadi nzima ya watu, ambao wataendelea kuwa bila usalama wa chakula. Sekta nyingine kama vile makazi, maji, usafi, ulinzi na elimu zitahitaji pesa. Sehemu kubwa ya nchi haiwezi kufikika katika msimu wa mvua. Msimu wa mvua ukianza hatuwezi kusafirisha bidhaa kwenye ardhi, na hiyo ni changamoto kubwa. Suala jingine ni ukosefu wa usalama kisiasa, ambao bado tunaona kati ya Sudan na Sudan Kusini. Tumeona hali ikitengamaa kidogo tunapokaribia mwishoni mwa mwaka, lakini hali bado ni tete mno.”

Anasema idadi ya wakimbizi kutokaSudan inatarajiwa kuongezeka hadi laki tatu na hamsini elfu, huku ghasia za kikabila zikitarajiwa kuwalazimu hadi watu laki mbili kuhama makwao hapo mwakani.