Mtaalamu wa UM aendelea kutafiti mfumo wa udhibiti wa mipaka ndani ya EU

21 Novemba 2012

Suala la udhibiti wa mipaka ya nchi za Umoja wa Ulaya litakuwa ajenda ya kipaumbele wakati wa ziara ya mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wahamiaji, François Crépeau huko Ugiriki kuanzia Jumapili ijayo.

Akizungumzia ziara hiyo ya siku tisa, Crepeau amesema anakwenda Ugiriki kwa kuwa nchi hiyo imekuwa kituo muhimu kinachotumiwa na watu wengi wanaotafuta hadhi ya uhamiaji barani Ulaya kutokana na kwamba nchi hiyo ina mpaka wa pamoja na Uturuki na bahari ya Mediteraniani.

Crepeau atakutana na maafisa mbali mbali nchini Ugiriki wakiwemo wale wa serikali wanaohusika na udhibiti wa mpaka na uhamiaji, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Ugiriki, mashirika ya kimataifa, taasisi zisizo za kiserikali na wahamiaji wenyewe ambapo watajadili udhibiti mkali wa mpaka wa Ugiriki.

Halikadhalika Mtaalamu huyo wa haki za binadamu atatembelea vituo ambako wahamiaji wanashikiliwa.

Tayari Bwana Crépeau’s ameshatembelea Ubelgiji, Tunisia na Uturuki na matokeo ya ziara hizo yatajumuishwa kwenye ripoti maalum itakayowasilishwa kwenye Baraza la haki za binadamu la umoja wa Mataifa mwezi juni mwakani.