Fedha zaidi zahitajika kwa ajli ya msaada wa chakula Madagascar kabla ya kimbuga: WFP

20 Novemba 2012

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema uhaba wa fedha ulisababisha lishindwe kuandaa kiwango cha kutosha cha msaada wa chakula kwa ajili ya wakazi wa maeneo yaliyoko kwenye mkondo wa kimbunga huko Madagascar.

Msemaji wa WFP Elizabeth Byrs amesema kutokana na hali hiyo wanaomba wahisani dola Milioni Sita nukta Moja kwa ajili ya msaada huo na kwamba shirika hilo litahitajika kuchangisha dola Milioni 15 katika kipindi cha miezi Sita ijayo kwa ajili ya miradi inayoendelea sasa ya kusadia watu zaidi ya Laki Tisa.

Watu hao ni pamoja na watoto wa shule walio katika mazingira magumu wakiwemo yatima na familia zilizoathiriwa na majanga asili na magonjwa kama vile Ukimwi na Kifua Kikuu.

Bi. Byrs amesema WFP inahitaji kuandaa zaidi ya tani Elfu Moja kabla ya kimbunga ambacho msimu wake ni mwezi huu wa Novemba.

Tunahitaji fedha ili kuandaa chakula cha kutosha kwa kutambua kuwa msimu wa kimbunga unaanza huko Madagascar mwezi Novemba. Kwa hiyo ni hali mbaya sana Madagascar ilikumbwa na vimbunga 50 katika miaka Kumi. Kwa hiyo ni muhimu sana na ni nchi maskini sana.

Bi. Byrs amesema iwapo hawatapata fedha hizo, WFP italazimika kusitisha baadhi ya miradi yake ya misaada ya chakula ifikapo mwezi ujao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter