UM wakaribisha mchakato wa amani Myanmar

20 Novemba 2012

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu nchini Mynmar amekaribisha aamuzi wa serikali ya nchi hiyo iliyohaidi kuendesha mageuzi yenye shabaha ya kuleta usawa na kuzingatia masuala yanayohusu haki za binadamu.

Tomás Ojea Quintana amesema kuwa uamuzi wa serikali ya Myanmar iliyokubali kupitia upya baadhi ya vifungu na sheria zake ikiwemo zile zinazohusu watu waliogerezani ni hatua ambayo inatia matumaini na haipaswi kupuuzwa na upande wowote.

Serikali ya Myanmar imesema kuwa itaanzisha chombo maalumu kwa ajili ya kupitia na kurekebisha sheria ikiwemo zile zinazowabana wafungwa walioko magerezani. Hatua hiyo inatazamiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi disemba.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa pamoja na kupongeza hatua hiyo lakini pia ametaka mashirikiano ya pamoja ili kufanikisha mpango huo ambao pia unatazamia kumulika ghasia zilizolikumba jimbo la Rakhine .