Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aung San Suu Kyi akubali jukumu la UNAIDS la kupinga unyanyapaa dhidi ya wenye Ukimwi

Aung San Suu Kyi akubali jukumu la UNAIDS la kupinga unyanyapaa dhidi ya wenye Ukimwi

Mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na Ukimwi, UNAIDS umemteua mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi kuongoza harakati za dunia za kupinga vitendo vya unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Taarifa ya UNAIDS inasema tayari Bi. Suu Kyi amekubali jukumu hilo wakati wa mkutano hivi karibuni kwenye makazi yake huko Nay Pyi Taw, Myanmar, kati yake na Mkurugenzi Mtendajiwa UNAIDS, Michel Sidibe.

Bi. Suu Kyi amesema anasikia fahari kuteuliwa kutetea na kuwa msemaji wa watu ambao wanatoswa na jamii katika harakati zao za kila siku za kuhakikisha wanaishi maisha yenye hadhi na kwa mujibu wa haki za binadamu.

Katika utekekelezaji wa jukumu hilo, atashawishi raia wa Myanmar na wakazi wa dunia yote wapinge vitendo vya unyanyapaa vinavyowakumba watu wenye virusi vya Ukimwi au Ukimwi.