Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji endelevu na wa usawa wahimizwa kwenye siku ya viwanda Afrika

Ukuaji endelevu na wa usawa wahimizwa kwenye siku ya viwanda Afrika

Ukuaji endelevu, wenye usawa na ambao unawahusisha wote unahitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia na malengo ya kichumi na kijamii ya ushirikiano wa maendeleo barani Afrika, NEPAD. Huo ndio ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, leo kwenye siku ya viwanda barani Afrika.

Bwana Ban amesema mwaka huu, siku ya viwanda barani Afrika inamlikia mchango muhimu wa biashara baina mataifa ya Afrika katika kupunguza umaskini, kuongeza usalama wa chakula na lishe na kusaidia kuleta maendeleo endelevu.

Bwana Ban amesema nchi za Afrika ni miongoni mwa zile zinazokuwa kwa kasi sana duniani, lakini biashara baina ya nchi hizo ni asilimia 10 tu ya biashara ya baraza zima, ambayo ni chini sana ikilinganishwa na maeneo mengine. Amesema kuna vizuizi vingi dhidi ya kupanua biashara barani Afrika, vikiwemo miundo mbinu duni, uwezo mdogo wa uzalishaji, ufadhili mdogo wa uwekezaji na gharama ghali ya kufanya biashara.

Ameongeza kuwa ikiwa bara la Afrika litataka kudhihirisha uwezo wake kikamilifu na kukabiliana na changamoto zake za kijamii, kiuchumi na maendeleo, ni lazima vizuizi hivi viondolewe.