Mapigano yalazimu huduma za kibinadamu kusitishwa Goma, DRC

20 Novemba 2012

Mashirika ya kutoa huduma za binadamu yamesitisha kwa muda oparesheni zake kwwenye maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati mapigano yanapochacha mjini Goma na vitongoji vyake. Mashirika mengi yanayotoa huduma nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yana vituo vyao mjini Goma.

Mapigano yamechacha kwa muda wa juma moja lililopita ambapo wanachama wa kundi la waasi la M23 wanapigana kuudhibiti mji wa Goma. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa mapigano yamevuruga huduma za kibinadamu huku wafanyikazi wa kutoa misaada nao wakilengwa. Mapigano hayo pia yamewalazimu watu 60,000 waliokuwa wakiishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kanyaruchinya kuikimbia kambi hiyo. Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

"Kwa sasa tuna wasiwasi na hali ilivyo mjini Goma ambapo watu zaidi wamehama kwa siku chache zilizopita. Kusonga mbele kwa waasi wa M23 kumewalazimu watu wengi kukimbia wakielekea mjni Goma na wengine Rwanda. Kwenye maeneo yanayouzunguka mji wa Goma wanawake na watoto wanaripotiwa kukusanyika eneo la Mugunga na sehemu zingine. Huduma nyingi za kibinadamu zimefutiliwa mbali kutokana na hali ya usalama iliyopo.Tangu mwanzo wa mwaka huu, mapigano mapya kwenye sehemu hizi mbili yameongezeka na kuwalazimu karibu watu 650,000 kuhama".