Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israeli na Hamas zisitishe mapigano na ziheshimu haki za binadamu za kimataifa:Ban

Israeli na Hamas zisitishe mapigano na ziheshimu haki za binadamu za kimataifa:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaendelea na ziara yake Mashariki ya Kati yenye lengo la kupatia suluhu mzozo kati ya kikundi cha Hamas na Israeli ambapo hii leo amesisitiza tena azma yake ya kuwa mapigano yanayoendelea kati ya pande mbili hizo huko Ukanda wa Gaza hayatafanya upande wowote kuwa salama.

Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Cairo, Misri mkutano ambao pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu Nabil Elaraby.

Ameeleza kwa raia wa Palestina na wale wa Israeli wanaishi kwa hofu ya kile kitakachotokea baada ya shambulio lingine na hali hiyo inapaswa kukomeshwa na kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kuzuia mapigano ya kutokea ardhini ambayo yatasababisha madhara makubwa zaidi.

Amesifu hatua za Umoja wa nchi za kiarabu za kuhamasisha harakati za kidiplomasia zinazoongozwa na Misri ili kusitisha mapigano huko Ukanda wa Gaza.

Katika mkutano huo pia Bwana Ban amezungumzia mzozo wa Syria na kuelezea wasiwasi waku kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na mapigano yanayoendelea ambayo amesema yanaweza kubadili Syria kuwa uwanja wa vita kwenye eneo hilo.

Bwana Ban akitoka Cairo amesema ataenda Israeli na baadaye Ramallah katika jitihada za kupatia suluhu mapigano huko Ukanda wa Gaza.