Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu huko Goma vyakithiri: UM

20 Novemba 2012

Mkuu wa Tume ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama na ukiukwaji wa haki za binadamu huko Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Msemaji wa tume hiyo, Rupert Colville amemkariri Bi. Pillay akisema kuwa kitendo cha waasi wa M23 kusonga kwenye mji wa Goma, kimetanguliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji, mateso kwa raia na uharibifu wa mali za watu.

Ameongeza kuwa M23 wamekuwa wakiwalenga raia kwenye mji huo wa Goma na viunga vyake kwa kuwa raia wanakataa kujiunga na kikundi hicho cha waasi.

Tume hiyo ya haki za binadamu imesema kuwa kikundi kilichokuwa kiende Goma kuangalia kiwango cha ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye eneo hilo, kililazimika kusitisha safari yake kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya zaidi.

Bi. Pillay amezitaka pande zote kwenye mzozo huo kuhakikisha wanalinda raia na mali zao.