Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuimarika kwa amani Yemen; Katibu Mkuu apongeza serikali na wananchi

Kuimarika kwa amani Yemen; Katibu Mkuu apongeza serikali na wananchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema Yemen ishikilie vyema maendeleo ya amani yaliyopatikana nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa makubaliano yaliyosaidia kumaliza ghasia nchini humo na kuelekea kwenye kipindi cha mpito cha demokrasia.

Bwana Ban amesema hayo mjini Sana’a, Yemen wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na viongozi wa nchi hiyo na makundi mbali ya kijamii na kidiplomasia, mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Rais wa Yemen Abdrabuh Mansour Hadi.

Amesifu jitihada zilizochukuliwa na nchi hiyo katika kipindi hiki cha mpito cha kuelekea kwenye amani baada ya vuguvugu la mabadiliko ambapo amesema mwaka mmoja uliopita kidogo Yemen ingetumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini kutokana na uongozi thabiti na ujasiri wa kisiasa Yemeni imebakia imara.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa utashirikiana na Yemen kuhakikisha inafanikiwa kidemokrasia na inastawi kwa manufaa ya wananchi wote na kamwe nchi hiyo isirudi nyuma.

Serikali ya umoja wa kitaifa nchini Yemen iliundwa mwezi Februari mwaka huu baada ya uchaguzi uliofanyika kufuatia makubaliano ya mwezi Novemba mwaka jana huko Riyadhi kati ya pande zilizokuwa zinakinzana.