Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za pamoja zahitajika kukabiliana na uharamia: Eliasson

Jitihada za pamoja zahitajika kukabiliana na uharamia: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesisitiza umuhimu wa mataifa yote duniani kushirikiana kukabiliana na vitendo vya uharamia ili kuhakikisha usalama wa mabaharia, wavuvi, abiria na wakati huo huo kulinda sekta ya utalii na uvuvi.

Bwana Eliasson amesema hayo leo wakati akitoa taarifa mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kuhusu uharamia na tishio lake kwa amani na usalama duniani, taarifa ambayo alitoa kwa niaba ya Katibu Mkuu Ban Ki-Moon. Amesema uharamia unaathiri uhuru wa usafirishaji majini, usalama wa meli ambazo husafirisha asilimia 90 ya bidhaa zote zinazohusika kwenye biashara ya dunia.

Akiwasilisha ripoti ya Bwana Ban kuhusu uharamia kando mwa pwani ya Somalia, Bwana Eliasson amesema vitendo vya uharamia kwenye pwani ya Afrika Mashariki vimepungua ikilinganishwa na mwaka jana. Hata hivyo amesema hatua lazima zichukuliwe kudhibiti matukio hayo.

(SAUTI YA ELIASSON)

Hali ya awali inaweza kurejea kwa urahisi iwapo sababu za uharamia kama vile ukosefu wa utulivu, ukosefu wa sheria na utawala bora havitashughulikiwa bila kusahau maendeleo muhimu ya kisiasa yaliyotokea hivi karibuni nchini Somalia. Ijapokuwa uharamia ni tatizo la dunia nzima, linatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kando mwa pwani ya Somalia maharamia wenye mbinu wanateka meli na wafanyakazi ili walipwe fedha ndio wawaachie. Huko ghuba ya Guinea, uharamia unahusiana na uporaji wa meli za mafuta unaohusishwa na soko haramu la mafuta kwenye ukanda huo na uhalifu. Kuna pia tofauti za kisiasa na utawala ambazo zimechangia ongezeko la uharamia kweney maeneo haya.”

Takwimu za shirika la usafirishaji majini duniani, IMO, tangu mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu kulikuwepo na matukio 291 ya uharamia na hadi sasa mabaharia 293 wanashikiliwa na maharamia hao huku maeneo yaliyoathirika zaidi yakiwa ni Afrika Mashariki, Afrika Magharibi na Mashariki ya mbali.