Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wasisitiza azimio la haki za binadamu la nchi za ASEAN likidhi vigezo vya kimataifa

UM wasisitiza azimio la haki za binadamu la nchi za ASEAN likidhi vigezo vya kimataifa

Mkuu wa Tume ya Haki binadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay amesifu hatua ya Umoja wa nchi za kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN ya kuridhia azimio la haki za binadamu huku hata hivyo akieleza wasiwasi wake kuwa nyaraka hiyo imetumia baadhi ya maneno ambayo yanaifanya isikidhi viwango vya kimataifa.

Kauli ya Pillay imekuja baada ya nchi za ASEAN kuridhia azimio hilo huko Phnom Penh Cambodia ambapo katika taarifa yao viongozi hao wameahidi kulinda na kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa katiba ya kuanzisha Umoja wa Mataifa na nyaraka zingine za kimataifa ambazo nchi hizo zimeridhia.

Amesema ni muhimu ASEAN ikahakikisha kuwa maneno yoyote yasiyoendana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu hayawi sehemu ya makubaliano yoyote kikanda kuhusu usimamizi wa haki za binadamu.

Bi. Pillay amesema mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu utaendelea kuwajibisha nchi za ASEAN juu ya haki za binadamu na kuzihamasisha nchi hizo kuimarisha zaidi muundo wao wa kusimamia haki za binadamu.