Uzalishaji wa mchele unazidi matumizi yake: FAO

19 Novemba 2012

Uzalishaji wa mchele kote duniani kwa mwaka 2012 unabashiriwa kuwa utazidi matumizi yake kati ya mwaka huu na mwaka ujao, na hivyo kuwepo tani milioni tano zaidi za nafaka hiyo inayotegemewa na wengi mwaka wa 2013, limesema Shirika la Chakula na Kilimo, FAO.

Kwa mujibu wa chombo cha kufuatilia soko la mchele, RMM, maghala ya mchele yanatarajiwa kujaa kwa hadi asilimia 7 zaidi, na hivyo kuongeza kiasi cha mchele duniani na kufikia takriban tani milioni 170. Mnamo mwezi Julai mwaka huu, FAO ilibashiri kiasi cha mchele unaozalishwa kupanda kwa tani milioni 4.2, kwa sababu ya hali nzuri ya hewa katika nchi za India, Misri, Jamhuri ya Korea, Ufilipino, Marekani na Viet Nam, ingawa ukame uliathiri uzalishaji katika nchi za Myanmar, Colombia na Senegal.

Ongezeko hilo linaonyesha miaka minane mfululizo ya kuongezeka kiasi mchele. Kufikia mwaka 2013, inatarajiwa kuwa kwa kila asilimia 34 ya matumizi, kutakuwa na ongezeko la asilimia 36 za uzalishaji.

Kuongezeka kwa uzalishaji katika bara Asia kunamaanisha kuwa sasa bara hilo ambalo hutumia zaidi mchele halitahitajika kuagiza chakula hicho kutoka ng’ambo kwa wingi.