Wakimbizi zaidi wa Sudan wawasili makazi ya Yida Sudan Kusini

16 Novemba 2012

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema katika kipindi cha wiki mbili sasa zaidi ya wakimbizi Elfu mbili wa Sudan wamewasili katika makazi ya Yida kukwepa mapigano nchini mwao.

UNHCR limesema hivi sasa watumishi wake wanafuatilia njia ya kwenda mpakani na wanasafirisha wakimbizi walio hatarini zaidi kuelekea kambi hiyo ya Yida na kwamba linajenga kituo cha kupata maji ili wakimbizi hao wawe na maji safi na salama.

Msemaji wa shirika hilo Adrian Edwards amesema kuna ongezeko kubwa la wakimbizi kuingia eneo hilo kwa sababu mapigano yamekuwa makali huko Kordofan Kusini.

Amesema zaidi ya asilimia 85 ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto ambapo wengi wao wamechoka kutokana na kutembea kwa siku kadhaa.

Bwana Edwards amesema tayari watoto 99 wenye umri chini ya miaka mitano wamebainika kuwa na utapiamlo na wanapatiwa huduma ya afya.

Halikadhalika amesema wakimbizi hao hupatiwa msaada wa dharura kama vile chakula na vifaa vya kubebea maji ili waweze kuishi vizuri kwenye makazi hayo ya muda.