Utoaji chanjo dhidi ya homa ya Manjano Sudan kuanza tarehe 24 mwezi huu: WHO

16 Novemba 2012

Kundi la kimataifa la kuratibu masuala ya chanjo, ICG limekubali ombi la serikali ya Sudan la kusaidia chanjo kwa ajili ya kinga dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano uliolipuka kwenye vitongoji 23 vya jimbo la Darfur.

Ugonjwa huo umejikita katika maeneo ya Kati, magharibi, Kusini, Kaskazini na Mashariki mwa jimbo hilo ambapo hadi Jumanne watu 110 walikufa kwa ugonjwa huo na bado kuna wagonjwa 374.

ICG pamoja na kukubali kutoa chanjo zaidi ya Milioni Mbili na Laki Nne, pamoja na vifaa vya sindano, itagharimia operesheni hiyo ya utoaji chanjo.

Wizara ya afya ya Sudan imepitia upya mpango wake wa chanjo na kuamua opereheni ya chanjo itafanyika kwanza kwenye vitongoji 12 kuanzia tarehe 24 mwezi huu.

Tarik Jasarevic ni msemaji wa WHO:

Leo chanjo za kwanza zitawasili Sudan na imepangwa kuwa chanjo Milioni Mbili nukta nne zitapelekwa leo na ndege nyingine yenye chanjo itawasili jumapili.zoezi la chanjo litaanza tarehe 24 Novemba kwenye vitongoji 12 vyenye mlipuko wa ugonjwa huo huko Darfur.