Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia walindwe dhidi ya vitendo vya ngono kwenye maeneo ya migogoro: UM

Raia walindwe dhidi ya vitendo vya ngono kwenye maeneo ya migogoro: UM

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji wa kingono katika maeneo yenye migogoro, Zainab Hawa Bangura ameshutumu vikali matukio ya kubakwa kwa wanawake na watu kukatwa viungo vyao vya siri huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC.

Kauli ya Bi. Bangura inafuatia ripoti ya kuwepo kwa vitendo mbali mbali vya unyanyasaji hususan wa kingono kwenye jimbo la Kivu Kaskazini huko DRC, ripoti inayotokana na uchunguzi uliofanywa na ofisi ya pamoja na Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za binadamu kwenye eneo hilo kati ya Aprili na Septemba mwaka huu..

Amesema vitendo hivyo vimefanywa kwa misingi ya kikabila na vikundi vya waasi wenye silaha na ameonya kuwa vitendo hivyo husaidia kuchochea mashambulizi zaidi na visasi.

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ghasia yoyote ya kingono kwenye migogoro inatishia amani na ulinzi wa jamii yote na hukwamisha jitihada za maridhiano hata baada ya mizozo kumalizika.

Ameitaka serikali ya DRC kuchukua hatua za haraka kurejesha ulinzi na kuhakikisha inalinda raia dhidi ya ghasia za aina hiyo.