UM wataka machafuko yakomeshwe katika mzozo wa Israel na Palestina

15 Novemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameelezea kusikitishwa kwake kuhusu hali inayozidi kuzorota kusini mwa Israel na Ukanda wa Gaza, na ambayo imehusisha makombora kurushwa kiholela kutoka Gaza yakiilenga Israel, na mauaji ya kulenga ya mwanajeshi wa Hamas na jeshi la Israel.

Bwana Ban amerejelea ujumbe wake wa kulaani vikali mashambulizi ya makombora kutoka Gaza, na kuelezea matarajio yake kuwa Israel haitajibu kwa njia inayosababisha umwagaji damu mpya ambao utawaathiri raia na kueneza athari zake kwenye kanda nzima.

Hofu ya kuibuka vita kati ya Israel na Palestina inazidi kuongezeka, kufuatia machafuko kwenye ukanda wa Gaza yalotokana na operesheni za jeshi la Israel dhidi ya Hamas. Bwana Ban amefanya mazungumzo na Rais Mohamed Morsi wa Misri kuhusu hali hiyo tete inayoweza kuchochea machafuko zaidi, na haja ya kuzuia hali kuzorota zaidi.

Baraza la Usalama pia limeongeza sauti yake kwenye ujumbe huo wa kuzitaka pande zote kujizuia, na kukomesha machafuko, kwa mujibu wa taarifa ilotolewa na rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu, Balozi Hardeep Singh Puri wa India.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud