Ripoti mpya yaonyesha uhusiano kati ya maliasili na uwezo wa nchi kukopesheka: UNEP

15 Novemba 2012

Ripoti mpya iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mazingira, UNEP na washirika wake imebaini uhusiano kati ya uthabiti wa kiuchumi wa nchi ikiwemo uwezo wake wa kulipa au kurejesha madeni na uharibifu wa maliasili kama vile misitu, mazao ya samaki na ardhi.

Ripoti hiyo itakayowasilishwa Jumatatu ijayo wakati wa tukio maaluum huko London, Uingereza inaonyesha vile ambavyo uharibifu wa maliasili na hatari ya nchi kunasa kwenye mtego wa kununua maliasili hizo kwa gharama kubwa kunavyoweza kuongeza deni la nchi husika ambalo limechochea na kuongeza mdororo wa kiuchumi.

Katika ripoti hiyo iliyohusisha nchi tano, UNEP inaeleza kwa sasa kuna hatari kubwa kwa nchi kumaliza kabisa maliasili zake na kuanza utegemezi na hivyo kuondoa mifumo ya awali iliyotumia maliasili kama kigezo cha kukopesheka.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud