Wafanyakazi wa UM waliokufa wakiwa kazini wakumbukwa

14 Novemba 2012

Umoja wa Mataifa hii leo umefanya kumbukumbu ya mwaka kwa wafanyakazi wake waliokufa wakiwa kazini ambapo kipindi husika ni kati ya Novemba Mosi mwaka jana hadi Novemba 30 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliongoza shughuli hiyo akiungwa mkono na Rais wa Baraza kuu la Umoja huo na yule wa Baraza la Usalama pamoja na wafanyakazi wengine ambapo waliwasha mishumaa kwa kumbukumbu hiyo.

Katika hotuba yake Bwana Ban amesema wanaokumbukwa na umoja huo mwaka huu ni wafanyakazi wake 29 wakiwemo raia, wanajeshi na polisi waliokufa wakitekeleza majukumu yao kwenye 11 tofauti vya kazi.

"Wenzetu hawa wanawakilisha mataifa 16. Katika majina yao na historia zao tunaona simulizi kuhusu Umoja wa Mataifa: Watu kutoka kona mbali mbali za dunia na mazingira ya kawaida kabisa wakifanya kazi mbali na makwao. Wengine walitoka maeneo ambayo awali yalighubikwa na migogoro na walikuwa tayari kupeleka amani kwa wengine.”

Mara baada ya kumbukumbu hiyo, Bwana Ban alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuimarisha usalama wa wafanyakazi wake.

Amezitaka pia serikali kuzingatia wajibu wao wa kuwalinda watumishi wa huo wa mataifa na kuwafikisha mbele ya sheria wale wote wanaowasaka au kuwashambulia wafanyakazi hao.