Uwepo wa njia za kupanga uzazi ni suala muhimu la haki za binadamu:UNFPA

14 Novemba 2012

Zaidi ya wanawake milioni 220 hawana uwezo wa kufikia njia za kupanga uzazi wanazojichagulia kwa mujibu wa mfuko wa idadi ya watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA). Shirika hilo linasema kuwa ukosefu au kutopatikana kwa njia za kupanga uzazi vimesababisha wanawake na familia zao kutumbukia kwenye umaskini, kuwa na afya duni na kukabiliwa na ubaguzi wa kijinsia.

Kupitia kwa ripoti ya kila mwaka kuhusu idadi ya watu (UNFPA) inasema kuwepo kwa njia za kupanga uzazi ni sehemu muhimu ya haki za binadamu ambayo imetajwa kuwa yenye manufaa ya kiuchumi na kijamiii.

Dianne Stewart kutoka UNFPA anasema kuwa uwekezaji kwenye sekta ya upangaji uzazi kwenye nchi zinazoendelea utapunguza matumizi ya huduma wakati mama anapokuwa na mimba na pia wakati ameshajifungua kwa zaidi ya dola bilioni 11.

Hata kama kuna hawa wanawake milioni 222 ambao  mahitaji yao ya upangaji uzazi hajatekelezwa., hatuwezi kufanikiwa kama hatuwezi kuwajumuisha wanaume  na watoto wa kiume kwenye mazungumzo ya upangaji uzazi. Wanahitaji kushirikishwa kwenye maamuzi haya na wanahitaji kuelewa njia mbadala walizo nazo na majukumu yao katika kuzuia mimba isiyotakikana. Upangaji uzazi tunaamini unahusu njia zote ambazo unaweza kuzipata kwa hiari zikiwemo njia za kisasa zinazopatikana na pia za kitamaduni na za kiasili za kupanga uzazi. Wanawake  wanahitaji njia za kujichagulia na njia hizi zinastahili kuwa tayari kwao.