Mtaalam wa UM kuchunguza hali za haki za binadamu Japan kufuatia tetemeko la ardhi 2011

12 Novemba 2012

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa, Anand Grover, ataizuru Japan tokea Novemba 15 hadi 26 ili kufuatilia masuala yanayohusiana na haki ya kuwa na afya nzuri katika nchi hiyo, katika muktadha wa tetemeko la ardhi lililotokea mashariki mwa nchi hiyo mnamo Machi 2011.

Katika taarifa, Bwana Grover amesema atazingatia uhusiano kati ya haki ya kuwa na afya nzuri kwa watu walioathiriwa na hatua za dharura zilizochukuliwa katika kukabiliana na uharibifu ulotokana na janga hilo, tsunami na ajali za nyuklia.

Hii ndiyo ziara ya kwanza kufanywa Japan na mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa, ili kukagua utekelezaji wa haki ya kila mmoja kufurahia haki za kuwa na afya nzuri kimwili na kiakili.

Bwana Grover, ambaye anaizuru Japan kufuatia mwaliko wa serikali ya nchi hiyo, atawasili mjini Tokyo, na kusafiri kwenda Fukushima na Miyagi, na kukutana na wadau wote katika jamii ya nchi hiyo, wakiwemo maafisa wa serikali, wataalam wa afya, na wawakilishi wa umma.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud