Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi Mkuu wa WHO ataka hatua zaidi kudhibiti matumizi ya Tumbaku

Mkurugenzi Mkuu wa WHO ataka hatua zaidi kudhibiti matumizi ya Tumbaku

Mkutano wa tano wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku umeanza huko Seoul, Korea Kusini ambapo Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Dkt. Margaret Chan amesifu jitihada za nchi hizo za kutekeleza mkataba huo licha ya changamoto zitokazo kwa wafanyabiashara wa tumbaku.

Dkt. Chan ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mvutano kati ya serikali zinazohaha kulinda afya za raia wake na kampuni za tumbaku ambazo vinataka kulinda faida zao, mvutano ambao amesema umelazimu pande hizo kufikishana mahakamani.

Mkuu huyo wa WHO amesema kazi ni kubwa lakini inatia moyo kwa kuwa hata nchi zilizosaini mkataba huo zimeongezeka na kufikia 176 sawa na asilimia 90 ya nchi zote duniani huku akizipongeza Australia na Norway kwa maamuzi yao ya kuweka sheria kali dhidi ya matumizi ya tumbaku.

(SAUTI YA Dkt. CHAN)

Mkutano huo wenye ajenda 25 unatarajiwa kuzingatia itifaki inayosubiri kupitishwa ambayo inayolenga kutokomeza biashara haramu ya bidhaa zitokanazo na tumbaku.