Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu yaendelea kuzorota Syria huku ghasia zikiongezeka

Hali ya kibinadamu yaendelea kuzorota Syria huku ghasia zikiongezeka

Hali ya kibinadamu imezidi kuzorota huku machafuko nchini Syria yakiwa yameongezeka, kwa mujibu wa mratibu wa huduma za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika kanda ya Mashariki ya Kati, Radhouane Nouicer, wakati wa kongamano la kibinadamu kuhusu Syria, ambalo linaendelea mjini Geneva, Uswisi.

Afisa huyo wa Umoja wa mataifa amewaambia waandishi wa habari kwamba mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka, huku watu wakiendelea kulazimika kuhama makwao, au kuuawa, na hasara za kiuchumi pia kuongezeka.

Naye mratibu wa kikanda wa Shirika la Wakimbizi la UNHCR, Panos Moumtzis, amesema katika siku moja iliyopita, zaidi ya wakimbizi kumi na moja elfu wa Syria wamevuka mipaka na kuingia Uturuki, Lebanon na Jordan.

Aidha, afisa kutoka Shirika la Afya Duniani, Richard Brenan, amesema mzozo wa Syria unaathiri vibaya mno huduma za afya. Amesema maelfu ya watu wameuawa, na thuluthi tatu za hospitali nchini kuharibiwa.