Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada zaendelea kupata chanjo ya numonia itokanayo na bakteria na kirusi: WHO

Jitihada zaendelea kupata chanjo ya numonia itokanayo na bakteria na kirusi: WHO

Katika kuelekea kuadhimisha siku ya numonia duniani tarehe 12 mwezi huu, Shirika la afya WHO limesema kwa sasa kuna chanjo ya numonia inayosababishwa na bakteria pekee wakati asilimia 30 ya visa vya numonia duniani ni mchanganyiko wa maambukizi ya bakteria na virusi.

Tarik Jasarevic ambaye ni msemaji wa WHO ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo hivi sasa shirika hilo linajikita kutafuta tiba ya numonia inayotokana na virusi na bakteria.

(SAUTI YA TARIK JASAREVIC)

Wataalamu wamekubaliana kuwa kipaumbele ni kuorodhesha tiba mbali mbali zilizopo hivi sasa dhidi ya magonjwa yote ya uambukizo wa njia ya hewa ikiwemo numonia na kutafiti tiba nyingine ambazo zitasaidia kupunguza mzigo utokanao na ugonjwa wa numonia na magonjwa mengine ya njia ya hewa. Matokeo yatawasilishwa katika mkutano wa wakuu wa mashirika ya kimataifa ya utafiti utakaofanyika Disemba huko London.”

Wakati huo huo ushirikiano wa kimataifa kuhusu chanjo, GAVI umesema ifikapo mwishoni mwa mwaka huu zaidi ya watoto Milioni 13 watakuwa wamepatiwa chanjo dhidi ya numonia.