Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu ahuzunishwa na vifo vilivyotokana na tetemeko la ardhi Guatemala

Katibu Mkuu ahuzunishwa na vifo vilivyotokana na tetemeko la ardhi Guatemala

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema umoja huo uko tayari kusaidi jitihada zinazofanywa na serikali ya Guatemala ya kutoa misaada ya kibinadamu kufuatia tetemeko la ardhi lililokumba nchi hiyo jana na kusababisha vifo vya watu 48 na wengine 150 kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Umoja wa Mataifa amemkariri Bwana Ban akielezea kusikitishwa na tukio hilo ambalo hadi sasa watu wengine hawajulikani walipo na wengine wanahaha kutafuta hifadhi mitaani kutokana na hofu ya mitikisiko mingine.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia jitihada za serikali ya Guatemala ikiwemo kutafuta msaada wa jumuiya ya kimataifa iwapo unahitajika.

Tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa Saba nukta Nne katika kipimo cha richa lilitokea katika eneo la mpakani mwa Guatemala na Mexico.