Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha zaidi zahitajika kusaidia chakula na watoto waende shule nchini Mali: OCHA

Fedha zaidi zahitajika kusaidia chakula na watoto waende shule nchini Mali: OCHA

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA limesema hali ya kibinadamu nchini Mali si nzuri na kwamba watu Milioni Nne nukta Sita nchini humo bado hawana uhakika wa chakula.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa uwezo wa wakazi wa kaskazini mwa nchi hiyo kupata chakula nao pia unapungua.

Amekariri OCHA ikisema kuwa elimu bado ni changamoto kubwa kwa Mali ambapo maelfu ya watoto kaskazini mwa nchi hiyo hawawezi kwenda shule na kwamba zaidi ya shule 130 kusini mwa Mali zimeharibiwa kutokana na mafuriko ya mwezi Septemba na Oktoba.

OCHA imesema bado fedha hazitoshi kwa kuwa kati ya dola Milioni 108 nukta Nane zilizoombwa kwa mahitaji, ni asilimia 49 tu ya kiasi hicho ndio kimepatikana.