UNESCO yatoa mafunzo kusaidia uandaaji wa vipindi bora kuhusu Ukimwi

8 Novemba 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO linaendesha mafunzo ya siku tano kwa waandaji wa vipindi vya radio wa nchi za Afrika Mashariki kwa ajili ya kuongeza ubora wa vipindi vya elimu kuhusu kinga dhidi ya Ukimwi na kuimarisha ushirikiano baina ya Radio katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika mafunzo hayo yanayofanyika Sengerema, Mwanza nchini Tanzania waandaji wa vipindi wanapatiwa stadi mbali mbali ikiwemo uandaaji wa vipindi bora vya kuelimisha vijana na kuhusu Ukimwi na jinsia na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo uchapishaji wa habari na uwekaji wa vipindi vyenye sauti katika intaneti kama njia mojawapo ya kusambaza zaidi elimu ya kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Mkufunzi mkuu Rose Mwalimu akizungumza wakati akiwakabidhi washiriki vifaa vya kisasa vya kurekodi amesema vyombo vya habari vya kawaida na vile vya kijamii vinaweza kuwa na nguvu kubwa katika vita dhidi ya Ukimwi hususan barani Afrika.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki wameweza kubainisha radio ndani ya Afrika Mashariki ambazo wanaweza kubadilishana vipindi hivyo vya elimu kuhusu Ukimwi.

UNESCO Tanzania na Kenya ndio waandaji wa mafunzo hayo yanayoleta pamoja washiriki kutoka nchi mbili hizo za Kenya na Tanzania pamoja na Rwanda na Uganda.