Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa kipalestina watendewe haki: Kamishna Mkuu UNRWA

Wakimbizi wa kipalestina watendewe haki: Kamishna Mkuu UNRWA

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada na ulinzi wa wakimbizi wa kipalestina, UNRWA Fillipo Grandi ametaka suluhisho la haki kwa zaidi ya wakimbizi Milioni Tano wa kipalestina.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Grandi ameelezea pia wasiwasi wake mkubwa kwa hali ya usalama ya wakimbizi zaidi la Laki tano wa kipalestina walioko Syria wakati huu wa mzozo nchini humo.

Amesema wakimbizi hao pamoja na wafanyakazi wa UNRWA wanajikuta katikati ya mazingira ya mzozo na mapigano na hivyo ametaka wapatiwe ulinzi wa hali ya juu kwa kuwa baadhi yao pamoja na raia wa Syria wameuawa, wamejeruhiwa na hata kulazimika kukimbia makazi yao.

Bwana Grandi ameonya kuwa kitendo cha wakimbizi hao kuendelea kukata tamaa na kuhisi wamepuuzwa kinaweza kuwa na madhara makubwa iwapo hatua za kuhakikisha usalama wao hazitachukuliwa.