Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la udhibiti wa Intaneti lasisitizia usalama wa wanaharakati wa tovuti za Intaneti

Kongamano la udhibiti wa Intaneti lasisitizia usalama wa wanaharakati wa tovuti za Intaneti

Uhuru wa kuwa na usemi kupitia kwa njia ya Intaneti umepata uungwaji mkono wa dhati katika kongamano la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuhusu udhibiti wa mfumo wa Intaneti mjini Baku, Azerbaijan.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa kitengo cha uhuru wa kuwa na usemi na maendeleo ya vyombo vya habari, Guy Berger, amemlikia umuhimu wa mpango wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa waandishi habari na suala la uwajibikaji katika kuangazia usalama wa kujieleza kupitia kwenye Intaneti.

Amesema kuwa uvamizi wa tovuti, kufungwa kwa tovuti hizo, kuwadhulumu wanaotumia uhuru wao wa kujieleza kupitia njia ya Intaneti, kufuatilia kwa karibu wanachochapisha, vitisho na hata mauaji, ni baadhi ya hatari inayowakabili wanaotaka kujieleza kihuru kwenye tovuti za intaneti.

Ameongeza kuwa, kuna haja ya kutambua kuwa waandishi wa habari sio tu wale waliopata mafunzo ya kitaaluma, ili kufahamu ni akina nani wanakumbwa na hatari kutokana na kujieleza kupitia kwenye Intaneti , kwani sasa kila mtu anaweza kuchapisha maoni yake kwenye tovuti za kijamii.