Jumuiya ya kimataifa isaidie Libya kukabiliana na ukwepaji wa sheria: Bensouda

7 Novemba 2012

Mwendesha Mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, Fatou Bensouda ameitaka jumuiya ya kimataifa kusaidia Libya kuondoka na vitendo vya kukwepa kuchukua mkono wa sheria na badala yake kusimamia utawala wa kisheria.

Bi.Bensouda amesema hayo leo mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati akiwasilisha ripoti yake ambapo ameeleza kuwa serikali ya Libya imejizatiti kushirikiana na ICC na inashawishika kuongeza maradufu jitihada zake.

Ameonegoza kuwa Libya inakabiliwa na changamoto wakati huu wa kipindi cha mpito lakini amesisitiza kuwa haki inapaswa kubakia kuwa jambo muhimu la kipindi hicho.

"Naiomba Jumuiya ya kimataifa hususan baraza la Usalama kuongeza jitihada zake za kusaidia serikali ya Libya kwa njia ambayo inaweza kupambana na vitendo vya ukwepaji sheria na kuendeleza utamaduni wa utawala wa sheria. Naamini kuwa kwa kufanya kazi pamoja tunaweza kushughulikia vitisho vinavyokabili usalama wa Libya ndani na nje ya nchi hiyo, vitisho ambavyo vinasababishwa na vitendo vya uhalifu vya zamani na vya sasa.”

Halikadhalika, Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC ameisihi serikali ya Libya kukamilisha mkakati wake wa kushughulikia vitendo vyote vya uhalifu nchini humo na vile vya kukwepa mkondo wa sheria.