AMISOM yaongezewa miezi minne zaidi nchini Somalia

7 Novemba 2012

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza kwa miezi minne zaidi muda wa kuwepo nchini Somalia kwa vikosi vya kimataifa vya kulinda amani nchini humo, AMISOM.

Uamuzi huo umeazimiwa leo wakati wa kikao cha baraza hilo mjini New York Marekani ambapo muda wa awali wa wiki moja ulioongezwa wiki iliyopita ulikuwa unamalizika leo.

Rais wa Baraza hilo Hardeep Singh Puri amesema uamuzi huo unafuatia ombi la Umoja wa Afrika na unalenga kuwezesha vikosi hivyo kusaidia serikali ya mpya ya Somalia katika jitihada zake za kujenga amani wakati huu ambapo tayari imeshateua baraza jipya la mawaziri.

AMISOM iliundwa mwezi Januari mwaka 2007 na baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika na kupata mamlaka yake ya utendaji kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.