Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majaji wa ICC waamua Laurent Gbagbo ana afya ya kukabili mashtaka

Majaji wa ICC waamua Laurent Gbagbo ana afya ya kukabili mashtaka

Jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Kivita, ICC, limeamua leo Novemba 2 kuwa aliyekuwa rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo yu bukheri wa afya na hivyo anaweza kusimama mashtaka mbele ya mahakama hiyo. Majaji hao wataweka tarehe karibuni ya kusikiliza kuthibitishwa kwa mashtaka katika kesi dhidi ya Bwana Gbagbo.

Kwa mujibu wa uamuzi wa majaji hao, maandalizi yanayofaa yatafanywa ili kumwezesha kushiriki katika kusikiliza mashtaka dhidi yake. Miongoni mwa maandalizi hayo ni kama kuwa na vikao vifupi vya koti, kuwekewa vifaa vinavyofaa wakati wa mapumziko na uwezekano wa mshtakiwa kuomba radhi asiwepo katika baadhi ya vikao, au hata kabisa, ili afuatilie vikao hivyo kwa njia ya video. Jopo hilo litaamua ni maandalizi yepi hasa yanafaa kwa kuendesha mashtaka hayo, kwa kushirikiana na upande wa kujitetea na afisi ya usajili wa mashtaka.

Bwana Laurent Gbagbo anadaiwa kuwajibika binafsi kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukiwemo mauaji, ubakaji na ukatili mwingine wa kingono, utesaji na vitendo vingine vya kinyama katika ghasia baada ya uchaguzi nchini Ivory Coast, kati ya Disemba 16, 2010 na Aprili 12, 2011. Tarehe ya kusikilizwa thibitisho la mashtaka dhidi yake iliahirishwa kutoka Agosti 13, 2012, kufuatia ombi la mawakili wake kuwa Bwana Gbagbo hakuwa katika hali nzuri ya afya kumwezesha kufanya hivyo.