Mauaji ya Syria kwenye video huenda yakawa uhalifu wa kivita: OHCHR

2 Novemba 2012

Mauaji ya wanajeshi wa serikali ya Syria kwa kufyatuliwa risasi na vikosi vya upinzani, na ambayo yalinaswa kwenye video, huenda yakaainishwa kama uhalifu wa vita, kwa mujibu wa afisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadam katika Umoja wa Mataifa.

Afisi hiyo ya haki za binadam imetoa wito kwa pande zote katika mzozo wa Syria kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binadam na sheria ya kimataifa ya kibinadam, na kila upande ukumbuke kuwa hatimaye utawajibika.

Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu video ilotolewa hivi karibuni ikionyesha watu wakinyongwa nchini Syria, msemaji wa afisi hiyo, Rupert Colville amesema, ni vigumu kuhakiki video hiyo mara moja na kujua ni wapi imenaswa na ni nani wamehusika, lakini inahitaji kuchunguzwa, na itachunguzwa kwa karibu zaidi.

"Madai ni kwamba hawa walikuwa mateka wa vita, na kwa hiyo, unaonekana kama uhalifu mwingine wa kivita. Kwa bahati mbaya, hii ni mojawapo ya mauaji ya kihalifu ambayo yamerekodiwa, yakitekelezwa na makundi ya upinzani, na vile vile vikosi vya serikali na makundi yanayoviunga mkono, kama vile Shabbiha. Bila shaka, watawajibika. Kuna ushahidi mwingi kutokana na uhalifu kama huu ambao umekuwa ukifanyika. Na video hii, ikiwa itahakikiwa, basi huenda ikawa miongoni mwa ushahidi huo."

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud