Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM ataka mashauriano kati ya serikali na vyama vya kijamii Belarus

Mtaalamu wa UM ataka mashauriano kati ya serikali na vyama vya kijamii Belarus

Mtaalamu mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchiniBelarus, Miklós Haraszti ametaka kufanyika kwa mjadala wa wazi kati yake na serikali ya nchi hiyo pamoja na vyama vya kijamii wenye lengo la kuendeleza na kulinda haki za binadamu nchini humo.

Haraszti amesema hayo leo ikiwa ni siku anayoanza rasmi jukumu hilo alilokabidhiwa na Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa na amesema ana matumaini ya kusaidia kuimarisha haki za binadamu nchini Belarus.

Amesema hatua ya kwanza itakuwa kupanga mkutano na serikali ya Belarus kujadili njia za kubadilishana taarifa muhimu ili kufanikisha jukumu lake na kwamba kufungua njia za mawasiliano na serikali na wadau wengine husika ni muhimu ili kuwa na ripoti thabiti atakayowasilisha kwenye kikao cha Baraza la Haki za binadamu na kile cha Baraza Kuu mwaka ujao.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha utumishi wake amekuwa akishirikiana vyema na serikali ya Belarus na vikundi vya kijamii  na hivyo uzoefu huo unampa  matumaini ya kutekeleza vizuri zaidi jukumu lake la kushughulikia haki za binadamu nchini humo.