Maeneo ya Kati na Kusini mwa Sudan yakumbwa na Homa ya manjano

31 Oktoba 2012

Mkurupuko wa homa ya manjano umewaua watu 32 katika maeneo ya kati mwa Sudan na Darfur, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO. Tangu wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, jumla ya watu 84 wanakadiriwa kuathiriwa na ugonjwa huo.

Shirika la Afya Duniani linasema lilijulishwa kuhusu mlipuko wa maradhi hayo na wizara ya afya ya Sudan mnamo Oktoba 29. Juhudi za kuwapa watu chanjo kwa halaiki zinaendelea kufanywa, ili kuwapa kinga hasa wale waliomo hatarini zaidi katika eneo la Darfur.

Wizara hiyo ya afya pia imesema imefanya udhibiti wa mbu wanaosambaza ugonjwa huo kuwa suala la kipaumbele, pamoja na kuongeza ufahamu wa umma kuhusu jinsi ya kujikinga au kuzuia ugonjwa huo.

Homa ya manjano husambazwa na mbu, na haina tiba inayojulikana kuitibu homa hiyo, ingawa chanjo ndiyo njia inayojulikana kuwa muhimu zaidi katika kuzuia maambukizi. Matumizi ya chandarua na dawa za kuzuia mbu ni njia mojawapo za kudhibiti usambazaji. WHO inasema inashirikiana na wizara ya Afya Sudan na wadau wengine kuweza kuudhibiti ugonjwa huo haraka.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud