Kusitisha mapigano Syria ni muhimu kwa ajili ya amani ya kudumu: Eliasson

25 Oktoba 2012

Umoja wa Mataifa umeendelea kuisihi serikali ya Syria na vikundi vya upinzani nchini humo kukubaliana kusitisha mapigano kwa dhati, na kueleza kuwa kusitisha mapigano ni kiashiria chanya kuwa pande zote ziko tayari kupatia mzozo huo suluhisho la amani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema harakati za kupatia suluhisho la kisiasa zinaweza kufanikiwa iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano yatatekelezwa.

Bwana Eliasson amesema tishio la mgogoro huo kuenea eneo lote la Mashariki ya Kati sasa ni dhahiri na ameomba nchi zenye ushawishi na pande zinazopingana nchini Syria kuzishinikiza pande hizo kuacha mapigano na kuingia katika majadiliano.

Hatuna uhakika kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano yatadumu. Tunatumaini kuwa pande zote zitatambua umuhimuu wa kuacha mapigano na kwa kufanya hivyo watathibitisha kuwa wanahitaji suluhisho, tena suluhisho la amani kwa manufaa ya raia wa Syria. Lakini jambo muhimu zaidini kwamba kitendo hicho kitaweka mazingira ambamo mchakato wa kisiasa utawezekana. Iwapo ghasia zitaibuka tena tutahisi mkanganyiko tena ambao tumekuwa tukiuhisi kwa kipindi sasa juu ya kutokuwepo kwa umoja ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Iwapo baraza hilo halina umoja, inaonyesha udhaifu wa Katibu Mkuu na wawakilishi wake. Iwapo tuna maazimio thabiti yanayoungwa mkono na nchi wanachama tuna nguvu za kuzunguumza na kubadili maneno yetu kuwa vitendo.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter