Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakaribisha hatua ya Brahimi kuomba usitishaji mapigano Syria

Baraza la Usalama lakaribisha hatua ya Brahimi kuomba usitishaji mapigano Syria

Wanachama wa Baraza la Usalama wamekaribisha mchakato wa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi, wa kuomba mapigano na aina zote za ghasia kusitishwa wakati wa kipindi cha Siku Kuu ya Eid al-Adha.

Wamerejelea pia wito wa pamoja wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu kwa wadau wote wa kikanda na kimataifa kuunga mkono mchakato huo wa Bwana Brahimi, na kutumia ushawishi walio nao dhidi ya pande zote kwenye mzozo wa Syria ili kuwezesha utekelezaji wa ombi la Bwana Brahimi la kusitisha mapigano na aina zote za machafuko.

Wanachama wa Baraza la Usalama wametoa wito kwa makundi husika katika mzozo, hususan serikali ya Syria, kuitikia mchakato wa Bwana Brahimi, na kurudia wito wao kwa serikali hiyo iruhusu mara moja wahudumu wa kibinadamu kuwafikia watu wote wanaohitaji msaada bila vizuizi vyovyote, kama ipasavyo chini ya sheria ya kimataifa na kanuni za huduma za kibinadam.

Katika muktadha huo, Baraza la Usalama limetoa wito kwa mataifa wanachama kuchangia haraka mpango wa Umoja wa Mataifa wa utoaji misaada ya kibinadamu nchini Syria.