Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi Mahiga alaani mauaji ya mwandishi wa habari Somalia

Balozi Mahiga alaani mauaji ya mwandishi wa habari Somalia

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Augustine Mahiga, amelaani mashambulizi ya hivi karibuni yaliyowalenga waandishi wa habari nchini Somalia.

Mnamo siku ya Jumanne, mwandishi wa habari wa Universal TV, Ahmed Saakin Farah Ilyas, alipigwa risasi na kuuawa katika mji wa Las-Anod kwenye eneo la Sool. Mnamo tarehe 21 Oktoba, mwandishi habari mwingine, Mohamed Mohamud Tuuryare, wa mtandao wa Shabelle mjini Mogadishu alifyatuliwa risasi nab ado yumo hali mahututi.

Balozi Mahiga amesema kujaribu kuwanyamazisha waandishi wa habari kutakuwa na athari mbaya mno kwa jamii ya waandishi wa habari nchini humo, na kulaani vikali mashambulizi hayo.

Ametaka mashambulizi haya yakomeshwe mara moja, na uhalifu huo kuchunguzwa na mamlaka za Somalia na Somaliland, ili wahusika wafikishwe mbele ya mkono wa sheria, na kuahidi msaada wa Umoja wa Mataifa katika kuimarisha vyombo vya uchunguzi.

Somalia ni mojawapo wa mahali penye hatari zaidi duniani kwa waandishi wa habari, huku mwaka 2012 ukiwa umeshuhudia vifo kumi na sita vya waandishi wa habari, na wengine 20 wakiripotiwa kujeruhiwa.