Tushirikiane tumalize majanga yanayoonekana na yasiyoonekana: Ban

23 Oktoba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa ujumbe wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza utekelezaji wa ahadi ya umoja huo ya kusitisha vita na kupatia suluhu migogoro isiyoonekana kama vile chuki, njaa, magonjwa na uharibifu wa mazingira.

Siku ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa kila tarehe 24 ya mwezi Oktoba ambapo Bwana Ban amesema kuwa ili kufanikisha hilo na kupata suluhisho la kudumu, dunia inahitaji ushirikiano kwa kuwa hakuna mtu mmoja au nchi moja pekee inayoweza kumaliza changamoto zilizopo.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Hata hivyo tunaweza kufanikiwa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, watendaji wakuu, wanasayansi, wasomi, watoa misaada na viongozi wa kijamii. Hakuna kiongozi mmoja pekee, nchi au taasisi anaweza kufanya vitu vyote. Lakini kila mmoja wetu anaweza kufanya kitu Fulani. Pamoja kama washirika tunaweza kukabiliana na vitisho, tukashinda vita na kutokomeza umaskini.”

Katika salamu hizo pia Bwana Ban anakumbusha majukumu ya Umoja wa Mataifa katika sehemu mbali mbali duniani .

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Umoja wa mataifa siyo sehemu ya mikutano ya wanadiplomasia. Umoja wa mataifa ni mlinzi wa amani, hupokonya silaha vikundi vya kijeshi, ni mhudumu wa afya kwani husambaza dawa, hutoa huduma za kibinadamu kwa kusaidia wakimbizi, pia ni mtaalamu wa haki za binadamu kwa kusaidia haki itendeke.”

Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945 baada ya vita kuu ya pili ya dunia na sasa ina wanachama 193 na miongoni mwa malengo yake ni kulinda amani duniani na kujenga mahusiano ya kirafiki baina ya nchi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter