Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa Umoja wa Mataifa waghadhabishwa na kunyongwa kwa watu Iran

Wataalam wa Umoja wa Mataifa waghadhabishwa na kunyongwa kwa watu Iran

Wataalam watatu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadam nchini Iran, hukumu za kunyonga na utesaji, leo wameelezea kughadhabishwa na kunyongwa kwa Saeed Sedighi na watu wengine tisa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

Wataalam hao, ambao ni Ahmed Shaheed, Christof Heyns na Juan E. Menendez, wamelaani vikali mauaji hayo, na kuelezea kusikitishwa kwao na ripoti za watu wengine kuendelea kuzuiliwa jela, na ambao bado wanakabiliwa na hatari ya kunyongwa kwa makosa ambayo hayachukuliwi kama uhalifu mbaya zaidi.

Bwana Sedighi amenyongwa licha ya wito wa jamii ya kimataifa, wakiwemo wataalam huru wa Baraza la Haki za Binadam la Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Iran kutofanya hivyo. Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wametowa wito kwa serikali ya Iran kuitikia wito wa jamii ya kimataifa wa kutotekeleza mauaji zaidi kama hayo.