Adhabu ya kifo inazidi kuonekana kuwa ni mateso: UM

23 Oktoba 2012

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya mateso, Juan Méndez amesema serikali zinapaswa kufikiria iwapo adhabu ya kifo yenyewe imeshindwa kuheshimu hadhi ya binadamu, inasababisha mateso ya kifikra na kimwili.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York, Marekani, Mendez amesema mpaka sasa adhabu ya kifo imekuwa ikitekelezwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa lakini wakati umefika utaratibu mpya ukawekwa ili kufanya adhabu hiyo iepushe mateso.

Amesema ripoti yake inataka ainisho jipya la uhalali wa adhabu ya kifo na ameonya kuwa serikali zinapaswa kuchunguza upya taratibu zao kwa mujibu wa sheria ya kimataifa kwa sababu uwezo wao wa kuweka na kutekeleza adhabu ya kifo unapungua kwa kuwa adhabu hiyo inaendelea kuonekana ni mateso.

Bwana Méndez amesema licha ya kwamba sheria ya kimataifa haionyeshi misingi tofauti juu ya haki ya kuishi ya makundi kama vile wajawazito, watoto, wazee na watu wenye matatizo ya akili, bado kuna hali inayokubalika na nchi nyingi kuwa adhabu ya kifo katika hali hiyo ni mateso.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud