UM walaani shambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Guinea-Bissau

22 Oktoba 2012

Umoja wa Mataifa umelaani shambulizi lililotekelezwa dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Guinea-Bissau mnamo siku ya Jumapili, na kuelezea kusikitishwa na vifo vilivyotokana na shambulizi hilo.

Katika taarifa ilotolewa siku ya Jumatatu, Umoja wa Mataifa umesema unafuatilia kwa karibu hali ilivyo. Mwakilishi maalum wa ofisi ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Guinea-Bissau (UNIOGBIS), Joseph Mutaboba, amekuwa akiwasiliana na viongozi wa taifa hilo pamoja na jamii ya kimataifa, ikiwemo makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

UM umetoa wito kuwe na utulivu, na kutaka wote nchini Guinea-Bissau kusuluhisha mizozo waliyo nayo kwa njia ya amani. Umoja wa Mataifa pia umeahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Guinea-Bissau na wadau wengine wa kimataifa, hususan Muungano wa Afrika, jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) jumuiya ya nchi zinazoongea lugha ya Kireno (CPLP) na jumuiya ya nchi za Ulaya, EU, ili kutekeleza azimio la Baraza la Usalama namba 2048, ambalo linataka hatua zichukuliwe mara moja kurejesha uongozi wa kikatiba, ukiwemo uchaguzi wa kidemokrasia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud