Skip to main content

Ushirikiano wapaswa kuimarishwa wakati wa mabadiliko kusini mwa bara la Afrika: UM

Ushirikiano wapaswa kuimarishwa wakati wa mabadiliko kusini mwa bara la Afrika: UM

Naibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadam katika Umoja wa Mataifa, Catherine Bragg ametoa wito kwa nchi zilizo kusini mwa bara la Afrika kuimarisha ushirikiano katika juhudi za kuendeleza uwezo wa kujiandaa kwa ajili ya majanga na kukabiliana na uhaba wa chakula.

Bi Bragg ametoa wito huo wakati akihitimisha ziara yake ya siku tano kwenye eneo hilo, akisema kwamba uhaba wa chakula linaendelea kuwa tatizo la kila mara kusini mwa Afrika, hususan katika nchi za Lesotho, Malawi, Swaziland na Zimbabwe. Nchini Lesotho, thuluthi moja ya idadi nzima ya watu hawana chakula cha kutosha kula au kuuza, huku Zimbabwe ikiwa na watu milioni 1.6 wanaotarajiwa kutokuwa na usalama wa chakula

Katika eneo hilo zima, zaidi ya watu milioni 5.5 katika nchi 8 wanakumbwa na uhaba wa chakula kwa sababu ya majanga ya mara kwa mara kama ukame na mafuriko, pamoja na mfumko wa bei ya chakula, idadi ambayo inaonyesha ongezeko la asilimia 40 kutoka mwaka 2011. Bi Bragg ambaye amezitembelea nchi za Botswana, Afrika Kusini na Zimbabwe, amesema eneo hilo linakumbwa na hali ya dharura ya uhaba wa chakula, ingawa haijatajwa.