Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM kutafuta suluhu endelevu kwa mzozo wa eneo la Sahel: Eliasson

UM kutafuta suluhu endelevu kwa mzozo wa eneo la Sahel: Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema kuwa ni lazima serikali ya Mali isaidiwe kuunda na kutekeleza mfumo wa kisiasa ambao unakabiliana na chanzo cha mzozo wa taifa hilo. Bwana Eliasson amesema hayo wakati wa mkutano baina yake na viongozi wa Muungano wa Afrika, jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambao pia umehudhuriwa na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Sahel, Romano Prodi.

Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa azimio nambari 2071 la Umoja wa Mataifa linatoa uwezo kwa Umoja wa Mataifa kusaidia kupata suluhisho endelevu kwa taifa la Mali. Katika muktadha huo, ameongeza kuwa utawala wa Mali ni lazima usaidiwe kupanga na kutekeleza operesheni za kijeshi ambazo huenda zikahitajika kurejesha maeneo yanayotawaliwa na makundi ya kigaidi na wahalifu chini ya utawala wake, bila kuifanya hali ya kibinadamu kuzorota zaidi.

Bwa Eliasson ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa umedhihirisha kujitolea kwake kupata suluhu kwa mzozo wa eneo la Sahel kwa kumteua Bwana Romano Prodi kama mwakilishi wake katika eneo hilo. Amesema Bwana Prodi atashirikiana na wadau wengine kuunda mkakati kuhusu eneo la Sahel wenye lengo la kukabiliana na ugaidi, uhalifu wa kupangwa, usambazaji wa silaha, ulanguzi wa fedha na kuboresha udhibiti wa mipaka.