Mfumuko wa bei Syria waongezeka, bei za bidhaa muhimu zapanda: OCHA

19 Oktoba 2012

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA, imesema kuwa mfumuko wa bei nchini Syria ambako bado mapigano yanaendelea kati ya majeshi ya serikali na vikosi vya upinzani umeongezeka na kufikia silimia 36 mwezi Julai mwaka huuu.

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa taarifa hizo ni kwa mujibu wa Benki Kuu ya Syria na kwamba ongezeko hilo la mfumuko wa bei limesababisha bei ya bidhaa za msingi kupanda kwa karibu asilimia Mia Tatu.

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema linaendelea kusaidai watoto na familia zao zilizopoteza makazi kutokana na mgogoro nchini Syria wakati huu wanapojiandaa kwa msimu wa baridi kali.

Msemaji wa UNICEF, Marixie Mercado akizungumza Geneva, Uswisi, amesema sasa hivi shirika hilo linapanga kupata nguo za joto kwa ajili ya watoto Elfu Sabini na Watano, mablanketi kwa ajili ya watoto wachanga na vifaa vya joto kwa ajili ya shule.

Hata hivyo amesema bado UNICEF inakabiliwa na uhaba wa fedha ambapo hadi sasa imeweza kupata dola Milioni 90 tu kati ya dola Milioni 132 zilizoombwa kwa ajili ya shughuli zake Syria na ukanda huo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter