Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brahimi aonya kuhusu kuenea kwa mzozo wa Syria nje ya mipaka

Brahimi aonya kuhusu kuenea kwa mzozo wa Syria nje ya mipaka

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi, amesema kuwa nchi katika kanda ya Mashariki ya Kati zinafaa kufahamu kuwa mzozo wa Syria hauwezi kubakia ndani ya mipaka ya Syria daima, na kuonya kuwa mzozo huo ama utasuluhishwa au utaenea nje ya mipaka ya Syria na kummeza kila mmoja.

Bwana Brahimi ametoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beirut, Lebanon, baada ya kukutana na rais wa Lebanon na maafisa wengine wakuu wa serikali.

Katika taarifa ilosomwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky, Bwana Brahimi na viongozi wa Lebanon wamejadili kuhusu wito wa Katibu Mkuu wa Mataifa wa kusitisha mapigano nchini Syria, hatua ambayo inatakiwa kutekelezwa kwanza na serikali, na kuigwa na upinzani. Amesisitiza wito wa Katibu Mkuu kwa nchi zinazotoa silaha kwa wahusika wote katia mzozo wa Syria kukoma kufanya hivyo, imesema taarifa hiyo.