Tunaishi katika majira ya kuwajibika kisheria: Ban

17 Oktoba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameuambia mjadala wa hadhara wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu amani na haki kuwa, majira ya sasa dunaini ni ya uwajibikaji. Bwana Ban amesema viongozi wa kiimla na wababe wa vita ambao hutekeleza uhalifu hawawezi tena kuacha mamlaka na kupewa hifadhi salama ng’ambo bila kukabiliwa na mkono wa sheria.

Katibu Mkuu amezungumzia ufanisi ulofikiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalfu, ICC, katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, akisema kuwa kila mahakama hiyo inapoingilia kati kwenye kesi fulani, iwe imetokana na mapendekezo ya Baraza la Usalama au vinginevyo, hali hubadilika.

Amesema hali huenda itaendelea kubadilika hivyo, wakati kesi zikichunguzwa, waranti za kuwakamata washukiwa zikitolewa, na wahalifu hao kukamatwa na kupelekwa The Hague, kufunguliwa mashtaka, na kuhukumiwa, na kuongeza kuwa kuwa kila mmoja ameona umuhimu wa mahakama hiyo ya ICC inapofuatilia haki katika maeneo yote duniani.