Umoja wa Mataifa kusaidia zaidi juhudi za maendeleo barani Afrika: Jeremic

17 Oktoba 2012

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, amesema maendeleo ya bara la Afrika yanapaswa kuwa sehemu muhimu ya majukumu ya mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa. Bwana Jeremic amesema hayo wakati wa kufungua vikao maalum vya juma la bara la Afrika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, chini ya Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika, NEPAD.

Bwana Jeremic amesema bara la Afrika lina uwezo mwingi, na kama rais wa Baraza Kuu, atajitahidi kuona kwamba bara hilo linaendeleza mtindo wa kutafuta suluhu kwa matatizo yake lenyewe, akitaja mifano ya maendeleo ya kisiasa yalofanywa nchini Somalia, na mazungumzo yanayoendelea ya amani kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Hata hivyo, Bwana Jeremic ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya usalama na kibinadamu katika eneo la Sahel, akisema hali hiyo inahitaji kuzingatiwa kwa dharura. Amesema Umoja wa Mataifa ni lazima ulisaidie taifa la Mali kulinda uhuru na mipaka yake, kama ilivyo kwa mataifa mengine wanachama, yakiwemo nchi za Maziwa Makuu, eneo ambalo amesema linatia wasiwasi. Ameongeza kuwa malengo ya maendeleo ya milenia ni lazima yabaki kuwa nguzo ya kati ya mtazamo wa pamoja kwa ajili ya ufanisi, amani na usawa wa Afrika.

(SAUTI YA VUK  JEREMIC)

Naye Msimamizi Mkuu wa NEPAD, Ibrahim Mayaki, ameelezea umuhimu wa juma la bara la Afrika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

(SAUTI YA IBRAHIM MAYIKI)

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud