Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe maalum wa UM Somalia apongeza kupitishwa kwa Waziri Mkuu mpya

Mjumbe maalum wa UM Somalia apongeza kupitishwa kwa Waziri Mkuu mpya

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga amepongeza hatua ya bunge la nchi hiyo kumpitisha Abdi Farah Shirdon kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Somalia.

Wabunge wote 215 waliridhia Shirdon kuwa Waziri Mkuu ambapo Balozi Mahiga amesema kitendo hicho ni ushahidi tosha usio na utata kuwa Somalia inasonga mbele.

Halikadhalika amesema bunge hilo limebeba matumaini ya wasomali na hivyo Waziri Mkuu mpya kupitishwa bila kupingwa ni kiashiria cha kuanza kwa ushirikiano na kuaminiana kati ya mihimili hiyo miwili ya dola.

Balozi Mahiga ameahidi kushirikiana na Waziri mkuu huyo mpya wa Somalia katika kutekeleza vipambele vya serikali na mahitaji ya haraka kama yalivyoelezwa na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, huku akimtaka ateue bila kuchelewa baraza jipya la mawaziri kwa kuwa majukumu ni mengi na hakuna muda wa kupoteza.