Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yalaumu kuchelea utekelezaji makubaliano ya amani Darfur

UNAMID yalaumu kuchelea utekelezaji makubaliano ya amani Darfur

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa kimataifa wa kulinda amani katika jimbo lenye mzozo la Darfur nchini Sudan amelaumu upigaji hatua mdogo juu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya serikali na vikosi vya waasi na amezitolea mwito pande zote kufanya juhudi kugharimia hali ya usalama na amani ya eneo hilo.

Aïchatou Mindaoudou,anayeongoza ujumbe wa UNAMID ameitaka serikali ya Khartoum pamoja na vikosi vya waasi kuonyesha utashi wa kisiasa kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2011 ambayo pamoja na mambo mengine yalidhamiria kukomesha uhasama wa kisiasa.

Akizungumza kwenye kikao cha pili cha kamishna ya kushughulikia mkwamo huo, mwanadiplomasia huyo amezilaumu pande zote kwa kuendelea kupiga dana dana makubaliano hayo ya amani.

Amesema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na UNAMID inayohimiza pande zote kuweka kando tofauti zao na kukaribisha duru ya maelewano lakini hata hivyo amesema kuwa juhudi hizo zimeambulia patupu.

Amezitaka pande hizo kudhihirisha utashi wa kisiasa ili hatimaye utekelezwaji wa makubaliano hayo ya amani udhihirike kwa vitendo.